MNADHIMU wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, ameendelea kumwandama Rais
Jakaya Kikwete, akisema baadhi ya majaji aliowateua hawana sifa, na
kwamba viongozi wa serikali waliojitokeza kumpinga wameshindwa kujibu
hoja.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana katika ofisi
ndogo ya Bunge, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki
(CHADEMA), alisema kuwa alishatoa maelezo hayo hata katika Kamati ya
Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Brigedia mstaafu Hassan
Ngwilizi.
“Nilieleza jinsi rais alivyofanya uteuzi wa baadhi ya majaji pasipo
kupata ushauri wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Wamekuwa wakijibu
kiujumla, mimi niliwataja kwa majina yao na hata hili nilieleza katika
Kamati ya Ngwilizi ambayo taarifa yake haikuwekwa hadharani pasipo
sababu za kueleweka,” alisema.
Alisema wanaotaka kujibu hoja zake wanapaswa kuweka hadharani orodha ya
majina ya majaji waliopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kuanzia
mwaka 2005 wakati Rais Kikwete alipoingia madarakani.
Lissu aliwataja baadhi ya watu waliowahi kujitokeza kumjibu kuwa ni
Naibu wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, ambaye alisema kuwa serikali
ina taarifa hizo na itazifanyia kazi.
Alisema kuwa msimamo huo ulikubaliwa na waziri wake, Mathias Chikawe na
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ambao kwa nyakati tofauti
walisema kuwa, endapo serikali itachukua hatua ambazo alipendekeza
watakuwa wanaingilia uhuru wa mahakama.
Wengine waliojitokeza kujibu hoja yake ni Jaji Mkuu, Othman Chande na
Jaji Kiongozi, Faki Jundu ambao walisema kuwa tuhuma zilizotolewa
bungeni si za kweli.
Pia Rais Kikwete naye alikaririwa hivi karibuni akiwa jijini Arusha
ambapo bila kumtaja Lissu kwa jina, alisema kuwa majaji wanateuliwa kwa
kufuata utaratibu na wana sifa zinazostahili.
Ni kutokana na kauli hizo, Lissu alifafanua kuwa, katika hoja zake
alisema kuna baadhi ya majaji waliteuliwa bila kuwa na sifa maalumu kama
zilivyobainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara
109, kipengele cha 6, 7 na 8.
“Ibara hiyo ya 109 kipengele cha 6-8 kinasema; mtu anaweza kuwa Jaji
iwapo tu ana shahada ya sheria kutoka katika chuo kinachotambuliwa
kisheria, awe ameshakuwa hakimu, awe ameshakuwa wakili na kusajiliwa na
sifa zote hizo ziambatane na utumishi wa miaka kumi mfululizo.
“Lakini sifa zote hizo lazima mtu anayeteuliwa kuwa Jaji awe nazo kwa
miaka kumi mfululizo. Sasa badala ya kuzungumzia masuala hayo kwa ujumla
jumla, ningependa wanaonijibu watamke wazi wazi Jaji Mbaruku Salumu
Mbaruku alisoma chuo kipi na akapata shahada ya sheria iliyompa sifa ya
kuwa jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar kabla ya kuteuliwa kuwa jaji wa
Mahakama ya Rufaa hadi sasa,” alisema.
Alishangaa viongozi wanaojitokeza kumjibu akisema hata Katiba ya
Zanzibar 94 (3) inasema; ili mtu achaguliwe kuwa jaji, ni lazima awe na
shahada ya Chuo Kikuu.
“Huyu jaji ambaye anasoma sasa alipataje kuwa jaji kabla ya kuwa na shahada ambayo ndiyo sifa ya msingi?” alihoji.
Lissu aliwataja majaji wengine ambao wameteuliwa bila kuwa na sifa kuwa
ni Fatuma Masengi, ambaye kwa mujibu wa Lissu alikuwa Hakimu wa Mahakama
ya Mwanzo Singida na baadaye akawa Hakimu Mkazi kisha akaanza kujisomea
Chuo Kikuu Huria na kuhitimu mwaka 2003 na kuteuliwa kuwa jaji mwaka
2006.
Alihoji kuwa kama katiba inaelekeza mtu awe jaji ni mpaka awe amekuwa hakimu kwa miaka 10, huyu alipataje kuwa jaji?
Majaji wengine waliotajwa ni Latifa Mansoor, ambaye pamoja na kuwa na
shahada ya sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyotunukiwa 1993,
lakini alifukuzwa kwa udanganyifu na ubadhirifu akiwa mfanyakazi katika
Manispaa ya Ilala.
Kwamba baadaye alipoibuka mwaka 2008 aliteuliwa kuwa jaji wakati
hajawahi kuwa wakili, na kwa kuwa alifukuzwa katika utumishi wa umma.
Lissu pia alimlalamikia Rais Kikwete kwa kutumia vibaya madaraka yake
kwani anateua majaji wa mikataba, ambao wameshastaafu na kulipwa mafao
yao.
Aliongeza kuwa, majaji wengine waliteuliwa na Rais wakiwa wagonjwa ili
waweze kupata fursa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi, ambapo alimtolea
mfano Jaji Mwendwa Malecela kuwa tangu ateuliwe mwaka 2006 hajawahi
kusikiliza kesi hata moja. Badala yake Lissu alidai kuwa jaji huyo
huenda matibabu India tu.
Kufuatia utata huo, Lissu emeendelea kushikilia msimamo wake kuwa
anakusudia kupeleka hoja binafsi bungeni ili Bunge liweze kuchunguza
utendaji wa rais kuhusu uteuzi wa majaji.
Lissu alisema Bunge litaangalia kama rais ameteua majaji kwa mujibu wa
katiba au ameikiuka, na kwamba yeye ana uhakika kuwa rais amekiuka
katiba.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !