Headlines News :

Written By Unknown on Thursday 29 November 2012 | 01:46

 
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, amejitoa katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Habari za kuaminika zilizopatikana mjini Dar es Salaam jana, zinasema Jaji Chande amejitoa na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Bernard Luhanda, ambaye atashirikiana na Natalia Kimaro na Salum Massati, kusikiliza rufani hiyo namba 47/2012 ya mwaka 2012.

Hii ni mara ya pili, kwa Jaji kujiondoa, baada ya Jaji Mbarouk Salim Mbarouk kuwahi kujitoa.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Lema alikiri kupata taarifa za kujitoa kwa Jaji Chande.

“Nimepokea taarifa ya kujitoa kwa Jaji Chande, sijui sababu ni nini… hii ni mara ya pili kwa jaji kujitoa, najiuliza maswali mengi nakosa majibu, …unajua kesi hii si yangu, ni wananchi ambao wanashauku kubwa ya kutaka kujua hatma yangu,” alisema Lema.

Alisema baada ya kusikia taarifa hiyo, aliwasiliana na wakili wake Method Kimomogolo, ambaye alimthibitishia kujiondoa kwa Jaji Chande.

Rufaa hiyo itasikilizwa saa tatu asubuhi na jopo la majaji watatu, Nathalia Kimaro, Salum Massati na Jaji Benard Luanda wa Mahakama ya Rufaa.

Novemba 8, mwaka huu Mahakama ya Rufani ilimwamuru Lema kufanya marekebisho ya dosari za kisheria katika muhtasari wa hukumu ndani ya siku 14, kutokana na pingamizi lililowekwa na wajibu rufaa.

Mrufani huyo alishawasilisha rufaa hiyo upya, baada ya kufanya marekebisho na tayari imepangwa kusikilizwa wiki ijayo.

Awali rufaa hiyo ilikuwa ikisikilizwa na jopo la majaji watatu, Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, Jaji Salum Massati na Jaji Nathalia Kimaro, ambapo kwa wiki ijayo hatokuwepo Jaji Othman, nafasi yake itachukuliwa na Jaji Luanda.

Lema alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 5, 2012 kufuatia kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

Baada ya kushindwa, Lema alikata rufaa Mahakama ya Rufani, kupitia kwa wakili wake Method Kimomogoro kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, huku akitoa hoja 18 za kupinga hukumu hiyo.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

 
Designed and Bloggerized by | Tryphone Chasama Jr | 0719 625003/0765860437
Proudly powered by BONGO BLOG DESIGNERS
Copyright © 2012. HABARI BONGO - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template