
Jumatatu, Septemba 17, 2012 05:56 Na Mwandishi Wetu, Misungwi [Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda] Waziri Mkuu, Mizengo Pinda *Asema imejaa mchwa
wanaotafuna fedha za umma *Aagiza watendaji wake wapelekwe mahakamani
*Asisitiza itakosa madiwani hadi mwaka 2015 *Wananchi wamzomea
mwenyekiti hadharani WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ametangaza kusudio la
kuivunja Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, kutokana na
halmashauri hiyo kukabiliwa na kashfa za ufisadi. Uchafu wa halmashauri
hiyo umeanzia kwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Benard Polcyarp na
baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wanaokabiliwa na tuhuma za
kufuja fedha za miradi ya maendeleo. Mbali na Pinda kutangaza kuifuta
halmashauri hiyo kwa kukosa sifa, pia aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), mkoani Mwanza kuchukua hatua.
Pinda aliitaka TAKUKURU kuanza mara moja kuandaa mashitaka, kisha
kuwapeleka mahakamani watuhumiwa wote wa ufisadi katika halmashauri hiyo
yenye madiwani 36 wote kutoka CCM. Pinda alifikia uamuzi huo baada ya
kubanwa maswali mengi na wananchi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika
juzi mjini Misungwi. Katika mkutano huo wananchi hao walimtaka Pinda
awaeleze kuhusu hatima ya halmashauri hiyo na tuhuma nzito za ufisadi
zinazomkabili mwenyekiti wa halmashauri hiyo. Wananchi hao pia walitaka
kujua hatua zinazochukuliwa dhidi ya baadhi ya vigogo, wanaotuhumiwa
kutafuna mabilioni ya fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri
hiyo. Kabla ya Pinda kutangaza kusudio hilo la kuivunja halmashauri
hiyo, wananchi waliokuwa wamefurika katika mkutano huo wakimzomea
mwenyekiti wa halmashauri hiyo, baada ya kuitwa jukwaani na Pinda kwa
lengo la kuwasalimia wananchi. Mara baada ya Pinda kumtaja mwenyekiti
huyo, umati karibu wote ulianza kumzomea Polcarp huku baadhi yao
wakipiga miluzi na kumwita fisadi mkubwa anayeitafuna halmashauri hiyo
ya Misungwi. Wananchi wengine walisikika wakimtaka waziri mkuu aondoke
naye, kwani amewachosha kwa vitendo vyake walivyodai vya kuhujumu fedha
za miradi ya maendeleo. Pinda alianza kwa kusema. “Kabla sijazungumza
lolote, kuna mtu muhimu sana hapa amesahaulika kutambulishwa. Namuomba
mwenyekiti wa halmashauri ya hapa Misungwi aje jukwaani japo awasalimie
wananchi,” alisema. Kutokana na kauli hiyo, wananchi walianza kuzomea
mwanzo hadi mwisho wa kupanda na kushuka jukwaani kwa mwenyekiti huyo.
Akiwa jukwaani huku akizomewa na umati huo wa wananchi, mwenyekiti huyo,
alianza kwa kusema: "Misungwi oyeee!", akazomewa. Kisha akasema kwa
lugha ya kisukuma: "Nalibona mwasayaga gete, lakini unene naliho duhu,
(yaani naona mmekasirika sana, lakini mimi nipo tu). Akazomewa tena na
kushindwa kuendelea, huku baadhi ya watu wakisikika wakimwita fisadi,
aondoke, Edipo Pinda alipomtaka ashuke chini. Baada ya zomea zomea hiyo
kuonekana kushika kasi zaidi, waziri mkuu alilazimika kubadili utaratibu
wa hotuba yake, ambapo aliomba wananchi wanaochukizwa na vitendo vya
mwenyekiti huyo wanyooshe mikono juu ili awaone. Hapo wananchi wengi
walinyoosha mikono yao, kisha Pinda akaomba wananchi watano wapite mbele
waulize maswali, ambapo watu sita waliuliza maswali yakiwemo ya tuhuma
za ufisadi katika halmashauri hiyo. Miongoni mwa vigogo wanaotuhumiwa na
ufisadi huo mkubwa ni Polcarp mwenyewe na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri hiyo, Exavieri Tilweselekwa, ambaye baadaye waziri mkuu
aliagiza mkurugenzi huyo ashushwe cheo na ashitakiwe mahakamani kwa
tuhuma hizo nzito. Akizungumzia tuhuma hizo, Pinda aliyeonekana
kukasirishwa na tuhuma hizo, alisema halmashauri hiyo imeelemewa na
mchwa mkali unaotafuna fedha za maendeleo, kwani mwaka 2009/2010 ilipata
hati yenye shaka. Pinda alisema, mwaka wa fedha 2010/2011 halmashauri
hiyo chini ya mwenyekiti wake, Polcarp ilipata tena hati chafu, jambo
linalothibitisha kuwepo kwa ulaji mkubwa wa fedha unaofanywa na baadhi
ya vigogo wa halmashauri hiyo. Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeonesha wazi kuwepo kwa upotevu
mkubwa wa fedha za maendeleo wilayani humo. Pinda alisema madai ya
mwenyekiti huyo kuwa Mbunge wa Misungwi Charles Kitwanga kuingilia
ukaguzi huo, hayana ukweli wowote, kwani vyombo hivyo ni vikubwa na vina
heshima kubwa ndani na nje ya nchi. "Ripoti ya CAG na ile ya tume
maalumu zinatueleza ukweli wa tatizo hapa Misungwi lipo wapi. Mwenyekiti
wenu huyu amekuwa akifanya biashara na halmashauri yake kupitia kampuni
yake ya ujenzi. Kimaadili, kiuongozi na kisiasa ni jambo lisilokubalika
hata kidogo. "Kiongozi mzuri na makini huwezi kufanya hivyo, maana
lazima italeta mgongano tu wa kimaslahi. Ni dhahiri hapa Misungwi hakuna
kinachofanyika katika kusimamia maendeleo ya wananchi. Nataka TAKUKURU
ifanye kazi yake tena kwa haraka sana. Na wahusika wote wa ufisadi huu
wapelekwe mahakamani". "Swali la kujiuliza hapa. Kwa nini mwenyekiti
ufanyebiashara na halmashauri? Kama una kampuni yako kwa nini
usingetafuta mtu ukamuweka akawa ndiye mwenye kampuni badala ya wewe
mwenyewe?. “Je ukijipatia tenda ya ujenzi utajisimamiaje, na nani
atakuwajibisha?", alihoji kwa jazba Waziri Mkuu Pinda, wakati akijibu
swali la Victor Thomas, aliyesema mwenyekiti huyo hahitajiki tena
kuiongoza halmashauri hiyo. Alisema, kulingana na uwepo wa tuhuma hizo
dhidi ya mwenyekiti huyo, alimshauri zaidi ya mara mbili juzi katika
kikao cha ndani na madiwani wote wa halmashauri hiyo. Katika mazungumzo
hayo, Pinda alimshauri Polcarp ajiuzulu nafasi hiyo, lakini alikataa
ushauri wake ambaye ndiye mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa na Tawala
za Mikoa nchini (TAMISEMI). “Juzi (majuzi), Polcarp alinifuata kuja
kuongea na mimi. Lakini nilimshauri ajiuzulu nafasi yake akakataa.
Aliniambia Misungwi hakuna tatizo (wananchi wakazomea). “Akaniambia
kwamba anayesababisha yeye achukiwe na wananchi ni mbunge
(Kitwanga)...lakini mimi (Polcarp), nakubalika sana". Wananchi wakazomea
tena. "Mwenyekiti huyu amekataa ushauri wangu wa kumtaka ajiuzulu. Mimi
ndiye Bosi wake na ndiye mwenye kauli ya mwisho. Ngoja nirejee Dar es
Salaam na ndani ya muda mfupi kisheria nitaivunja halmashauri hii ya
Misungwi. "Itakuwa kama ile ya Dar es Salaam ilipovunjwa miaka ile ya
nyuma. Maamuzi haya ni mazito maana hapa Misungwi hamtakuwa na madiwani
hadi mwaka 2015, na hatua kali za kisheria lazima zichukuliwe kwa
wahusika wote", alisema Pinda huku wananchi wengi wakishangilia na
kumtaka aivunje halmashauri hiyo papo hapo, kwa madai wamechoshwa na
ufisadi. Miaka ya nyuma Serikali iliwahi pia kuivunja halmashauri ya Dar
es Salaam, baada ya kuwepo kwa tuhuma zinazofanana na zile za
halmashauri ya wilaya ya Misungwi, ambapo italazimika kuundwa tume
maalumu ya kwenda kusimamia shughuli zote za madiwani. Baadhi ya wakazi
wa wilaya Misungwi, walieleza kufurahiswa na maamuzi ya Pinda kuivunja
halmashauri hiyo ndani ya siku chache zijazo, na kwamba wamechoshwa na
baadhi ya vigogo wa halmashauri hiyo kutafuna fedha za miradi ya
maendeleo
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !